Tuesday, 8 December 2015

SUKARI KUTOKA NJE INAVYOUA VIWANDA VYA NCHINI


MTZ UCHUMI HII SAFI.inddMTZ UCHUMI HII SAFI.indd>>TPC wataka itozwe kodi ya asilimia 100
NA UPENDO MOSHA, MOSHI
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazoendelea Afrika kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi vikiwemo viwanda.
Licha ya umuhimu wa viwanda hivyo bado kumekuwa hakuna sera madhubuti zinazolenga kuboresha na kuendeleza
viwanda vya ndani.
Sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha kuchelewesha malengo yaliokusudiwa ya kukuza uchumi na maisha bora kwa wananchi wake.
Sera zilizopo zinaruhusu kuuzwa kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nje ya nchi na hata zile zinazozalishwa ndani lakini kumekuwa na tatizo katika bidhaa zinazozalishwa ndani.
Bidhaa ambazo zimeonekana kuteka masoko yetu nyingi zinatoka nje licha ya kwamba ziko bidhaa nyingi zinazozalishwa na viwanda vya ndani lakini zinakosa soko.
Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko, inaonyesha kuwa sekta ya viwanda nchini imekuwa ikikua kwa asilimia tisa tu kwa mwaka, kiwango ambacho bado ni kidogo.
Wawekezaji wa viwanda mbalimbali nchini wamekuwa wakiathiriwa katika uzalishaji kutokana na kutokuwapo kwa sera madhubuti ya kuvilinda viwanda vya ndani.
Na hii ni kutokana na baadhi ya sera hizo kuruhusu uagizwaji wa bidhaa sawa na zile zinazozalishwa hapa nchini na ambazo mara nyingi huuzwa kwa bei ya chini kuliko zinazozalishwa hapa nchini na hivyo kuathiri viwanda vya ndani.
Mojawapo ya viwanda vilivyothiriwa na hali hiyo ni Kiwanda cha kuzalisha sukari cha TPC kilichoko eneo la Langasani, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kiwanda hiki kimekuwa kikikabiliwa na changamoto kubwa ya kushindwa kuhimili misukosuko ya soko la ndani kutokana na uagizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi. Sukari hiyo inayoagizwa kutoka nje huuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na ile inayozalishwa hapa nchini.
Ofisa Utawala wa kiwanda hicho, Jaffary Ally, anasema kiwanda hicho kilibinafsishwa na Serikali mwaka 2000 na kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nchini Morishes, (Mauritius).
Anasema tangu kukabidhiwa kwa wawekezaji binafsi, kiwanda cha TPC kimepata mafanikio makubwa katika
uzalishaji lakini kimekuwa kikikumbana na changamoto ya kuathiriwa na sukari inayoagizwa kutoka nje ya nchi kiholela.
“Tumelalamika sana katika ngazi mbalimbali za uongozi hapa nchini kuhusiana na athari tunazokutana nazo
kibiashara kutokana na sukari inayoagizwa kutoka nje ya nchi na hali hii inazidi kuota mizizi,” anasema Jaffary.
Anasema sukari inayozalishwa nchini imekuwa ikishindwa kufanya vizuri katika soko la ndani kwa sababu Serikali
imeruhusu wafanyabishara kuingiza sukari kutoka nje ambayo haitozwi kodi inavyostahili.
Anasema sukari hiyo imekuwa ikiuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na sukari inayozalishwa na viwanda vya hapa nchini na kwamba hali hiyo imekuwa ikididimiza uchumi wa viwanda vya hapa ndani na ule wa Taifa kwa ujumla.
“Sukari hii imekuwa ikiingizwa nchini kiholela na kodi inayotozwa ni ile ya ongezeko la thamani (VAT), hivyo
imekuwa ikiuzwa kwa bei ya chini mno tofauti na sukari inayozalishwa hapa kwetu.
Inayozalishwa kupitia viwanda vya ndani imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu kutokana na gharama za uzalishaji,” anasema.
Anasema wawekezaji wa ndani wanahitaji kuwa na ushindani wa soko ulio wa haki hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa sukari hiyo inatozwa kodi zote zinazostahili.
Anasema viwanda vya sukari nje ya nchi huwa vinazalisha ya ziada na kupelekwa katika soko la dunia la sukari na
huko huuzwa kwa bei ya chini mno na inaponunuliwa huletwa hapa nchini na kuuzwa kwa bei ya chini na hivyo kuathiri viwanda vya ndani.
“Sukari hii wenzetu wanapoipeleka kwenye soko la dunia hairudi tena kwenye masoko yaliyomo kwenye nchi zao, baada ya kukusanya kodi, huongeza kiwango hicho cha kodi na kuwa kubwa kiasi cha asilimia 60 na 90, ili isirudishwe nchini mwao kwa vile bei itakuwa ni kubwa,” anasema.
Jaffary anasema sukari inayotoka nje ingepaswa kutozwa kodi asilimia 100 ili kulinda viwanda vya ndani.
“Cha ajabu ni kwamba kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita sukari inayotoka nje haijawahi kutozwa kodi hata asilimia 50 ili kulinda viwanda vya ndani, achilia mbali sukari inayoingia kwa magendo,” anasema.
Ofisa huyo anasema sukari ya magendo hailipiwi VAT wala kodi ya aina yeyote hali ambayo huathiri vibaya zaidi soko la ndani na kusababisha kuathirika kwa viwanda vya ndani.
Anasema viwanda vya ndani vina uwezo wa kuzalisha sukari inayotosheleza mahitaji iwapo tu Serikali itaweka mipango madhubuti ya kuvilinda viwanda hivyo.
Anasema ni vyema Serikali ikaweka utaratibu unaofaa wa sukari hiyo kuruhusiwa kuingia nchini katika misimu
ambayo viwanda vya ndani havizalishi.
“Sukari zije wakati viwanda vyetu vya ndani havizalishi kwani tumeshuhudia meli zinazoegeshwa pembezoni mwa bahari zikiwa zimehesheni sukari kutoka katika nchi za nje na wafanyabiashara wamekuwa wakifanya hujuma ya kupaki sukari hizo kwenye mifuko ya viwanda vyetu vya ndani ili ionekane imezalishwa hapa nchini”, anasema.
Anaishauri Serikali kuongeza nguvu zaidi ya kupambana na wafanyabishara wanaoingiza sukari hiyo kwa njia isiyokuwa halali.
Anasema mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani zaidi ya 400,000 ambapo viwanda vya hapa nchini vya TPC, Mtibwa, Kilombero na Kagera huzalisha zaidi ya tani 320,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo, kati ya tani hizo kiwanda cha TPC huzalisha tani 105,000 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya sukari yote inayozalishwa hapa nchini kwa mwaka.
Anasema wakati wanakabidhiwa kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa mwaka na kwamba Serikali iliwawekea malengo kutoka kuzalisha tani hizo hadi kufikisha tani 72,000 za sukari kwa mwaka.
Hata hivyo anasema licha ya changamoto zinazowakabili wamefanikiwa kuvuka lengo hilo na sasa wanazalisha zaidi
ya tani 100,000 kwa mwaka.
“Tumejiwekea malengo ya kuzalisha tani 120,000 katika miaka mitano ijayo iwapo Serikali itaweka mazingira ya kulinda soko la ndani,” anasema.
Anasema mbali na hilo pia kiwanda hicho kimefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa miwa ambapo ekari moja huvunwa wastani wa miwa zaidi ya tani 140 na kwamba kuna baadhi ya mashamba hutoa zaidi ya tani 200 kwa ekari.
“Kwa sasa TPC inajivunia mafanikio makubwa na iwapo Serikali itatoa fursa ya mazingira mazuri ya ushindani
tutakuwa na uwezo wa kushindana na hata kukishinda kiwanda chochote cha uzalishaji sukari barani Afrika na hata nje ya Afrika,” anasema.Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Robert Baizaki, anasema kwa sasa sukari imezidi kurundikana kwenye maghala kufuatia kuwapo wa sukari nyingi kutoka nje ya nchi.
“Ni vyema sasa Serikali ikadhibiti uingizwaji wa sukari kutoka nje kwa lengo la kunusuru wawekezaji na uchumi wa taifa kwa ujumla,” anasema Baizaki.
Kauli ya Serikali Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabishara wote wanaojihusisha na uingizwaji wa sukari kiholela kutoka nje. Makala anasema uingizwaji wa sukari za magendo unaathiri kwa kiasi kikubwa
wawekezaji wa ndani wanaozalisha sukari na kwamba Serikali mkoani humo haiko tayari kulivumilia suala hilo.
Mkuu huyo pia aliahidi kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Tanga ili kuwakamata wafanyabishara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiitumia bandari ya Tanga kuingiza sukari.
“Tutaweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi na kuwakamata wahusika watakaobainika kufanya hivyo,” anasema.


IMETOKA MTANZANIA

No comments:

Post a Comment