Tuesday, 24 November 2015

MAHAKAMA YAFYEKELEA MBALI PINGAMIZI LA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA LILE LA MKUU WA MKOA WA MWANZA







MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, jana ilishindwa kutoa maamuzi ya kesi iliyofunguliwa na familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita, Marehemu Alphonce Mawazo. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).
Kesi hiyo namba 10/2015 iliyopo chini ya Jaji, Lameck Mlacha, imefunguliwa juzi na familia hiyo ya Mawazo kwa lengo la kuomba tafsiri ya kisheria mahakamani hapo iwapo marehemu huyo hapaswi uzikwa kwa kuagwa kwa heshima kama wanavyoagwa binadamu wengine.
Awali leo mahakama hiyo ilisikiliza pande zote mbili za mlalamikaji na walalamikiwa, kisha kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa mahakamani na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kufuatia hali hiyo mahakama hiyo iliahirisha kwa muda kusikiliza shauri hilo kisha kutoa muda wa saa 1:30 kwa upande wa mlalamikaji ambayo ni familia ya Mawazo, kuwasilisha malalamiko muhimu mahakamani hapo.
Hata hivyo baadaye upande huo wa mlalamikaji uliwasilisha hoja hizo mahakamani hapo, ambapo Jaji Mlacha alidai baadhi ya vipengele vilikuwa havijakamilika, kwamba muda wa Mahakama hiyo pia ulikuwa umekwisha, hivyo kuipanga kesho kwa ajili ya kutoa maamuzi.
Hata hivyo, Jaji Mlacha aliwaacha solemba wananchi, wafuasia na viongozi wa Chadema baada ya kuamua kutolea maamuzi hayo sehemu nyingine mbali na Mahakama hiyo, hivyo kujikuta wananchi na wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamefurika kwa wingi mahakamani hapo wakipigwa butwaa.
Jaji Mlacha alitolea maamuzi hayo ya kuendelea kwa kesi hiyo kesho katika Ofisi yake iliyopo kwenye jengo la Mahakama Kuu ya Biashara Mkoa wa Mwanza.
Kesi yafunguliwa upya
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo leo jioni, mmoja wa mwanasheria wanaoitetea familia ya marehemu Mawazo, John Malya amesema familia hiyo imeamua kufungua kesi hiyo upya baada ya awali kuombwa na Mahakama hiyo kupeleka malalamiko mapya.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, kesi hiyo imefunguliwa tena leo kwa hati ya dharula ikiwa ni lengo la kuiomba Mahakama hiyo kutoa tafsiri ya kisheria kuhusu namna marehemu Mawazo anavyopaswa azikwe.
“Tunataka Mahakama itamke kwamba zuio lililowekwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (Charles Mkumbo) la kuzuia kuagwa Mawazo ni batili.
“Mahakama tunaiomba imkataze RPC kujihusisha na mazishi ya marehemu Alphonce Mawazo. Tunaamini Mahakama itatumia weledi wake kutenda haki katika kesi hii,” amesema mwanasheria Mallya.
Maamuzi ya awali
Awali Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ilitupilia mbali pingamizi mbili zilizowasilishwa mahakamani hapo baina ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza na Mwasheria Mkuu wa Serikali.
Pingamizi hizo zilidai mlalamikaji ambaye pia ni baba mdogo wa marehemu Mawazo, Charles Lugiko hana uhalali wa kisheria wa kutoa maombi hayo mahakamani, kwa kuwa yeye siyo baba mzazi wa marehemu Mawazo.
Kwamba hakuwasilisha mahakamani hapo hoja za kubishaniwa kwenye maombi hayo, jambo ambalo Jaji wa Mahakama hiyo, Lameck Mlacha aliziona pingamizi hizo zilizowasilishwa mahakamani hapo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hazina uzito kisheria.
Katika kesi hiyo namba 10/2015, familia ya marehemu Mawazo inawakilishwa na wanasheria wa Chadema ambao ni John Mallya, James Millya na Paul Kipeja, ambapo katika kujibu hoja hiyo ya upande wa walalamikiwa waliiambia Mahakama masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kupelekwa mahakamani.
Upande huo wa Jamhuri uliokuwa ukisimamiwa na wanasheria wawili, Seth Mkemwa na Emilly Kilia, awali ulidai kwamba mlalamikaji huyo hana uhalali wowote wa kupata ridhaa ya mahakama ya kumzika Mawazo, kwani hata katika maombi yake hajaonesha wazazi wa Mawazo kama wamefariki ama wapo hai.
Hata hivyo katika pingamizi hizo za awali, Jaji Mlacha alidai kwamba katika sheria namba 17 na 18 kifungu cha nne, vinaruhusu mtu yeyote aliyekuwa karibu na marehemu Mawazo anaweza kudai haki ya kumzika, kwani hata mila na desturi za kiafrika zinaeleza.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Jaji Mlacha, amesema kuwa hoja zinazotolewa na wanasheria wa Serikali wa kumpinga mlalamikaji kutosikilizwa mahakamani hazina tija, ambako alidai katika hati za mashitaka baba mdogo huyo alieleza kuwa alimlea na kumkuza hivyo anaowajibu wa kumzika
Upande wa mlalamikaji, uliokuwa ukitetewa na mawakili watatu, John Mallya, James Milya na Paul Kipeja, ulidai kuwa pingamizi za wanasheria wa Serikali ya kuomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo hazina msingi kwani mtu yeyote aliemlea marehemu anauwezo wa kuzika.
“Jaji amedai tupeleke maombi rasmi ya kutupilia mbali zuio la kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwaza Charles Mkumbo ya kuzuia kuagwa Mawazo hapa Mwanza, mambo tunayopeleka ni kutaka mahakama kutengua zuio la Polisi, Mahakama kumkataza RPC kutojihusisha na chochote kile kwenye kumuaga Mawazo,” alidai Mallya.
Mallya alidai kwamba katika maombi yao ya msingi wanayowasilisha mahakama ni ya kumzuia RPC Mkumbo kutojihusisha na chochote, huku akidai kwamba zoezi la kamanda huyo kuzuia uagaji lilikuwa ni batili na halikuwa halali.
Mbowe anena
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, akizungumza na umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza mahakamani hapo jana, ambapo aliwaomba wafuasi hao kuwa na subira kwani Mahakama itatoa uamuzi wakati wote wote.
Mbowe amesema Watanzania wote wakiwamo wapenda mabadiliko na watafuta haki nchini kuvuta subira kwani haki ya mtu haiwezi kunyang`anywa na watu wachache, kwa maslahi yao binafsi, kwani wana imani na Mahakama itatenda haki.
“Mpaka sasa tulipofikia tunaishukru Mahakama imeweza kufanya kazi yake. Tunaomba tuvumiliane na tuwe na subira, kwa sababu wanasheria wamepewa saa 1 na nusu wawe wamewasilisha maombi yao ya msingi ya kusikilizwa kesi hii na kutupilia mbali pingamizi wa wanansheria,” amesema Mbowe.
Watu wafurika mahakamani
Katika hatua nyingine, jana na leo maelfu ya wananchi walijitokeza kwa wingi kwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo la kikatiba, ambapo hata baada ya Mahakama kutupilia mbali pingamizi za Jamhuri, wananchi walionekana kushangilia kwa nguvu huku wakiimba nyimbo mbalimbali za chama hicho.
Pamoja na wananchi kujaa mahakamani hapo, maofisa wa Serikali wakiwamo askari polisi na maofisa wengine kutoka taasisi na idara za ulinzi na usalama nao walionekana kutanda kila mahala eneo hilo.
Askari polisi ambao wengi wao walikuwa wamevalia kiraia na wengine wakiwa na sare za jeshi hilo, walijaa mahakamani hapo kwa ajili ya kuimalisha ulinzi, ambapo hata hivyo hakuna vurugu zozote zilizotokea.
Baada ya Mahakama kutoa muda huo kwa upande wa walalamikaji kurekebisha baadhi ya vipengere vya kisheria, wananchi wengi wakiwamo wanawake, vijana na wazee walionekana kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama kutupilia mbali pingamizi hizo za RPC na AG.
Hata hivyo, wananchi hao wakiwamo wafuasi na viongozi mbalimbali wa Chadema walionekana kuwa watulivu baada ya Mwenyekiti Mbowe kuwasihi kupunguza munkari, hali iliyosababisha wengi wao kuanza kupongezana huku wakidai wameshinda kesi.
Baadhi ya viongozi na makada wa Chadema waliozungumza na MwanaHALISI Online kuhusu uamuzi huo wa awali, waliipongeza Mahakama kwa kutupilia mbali pingamizi hilo la upande wa Jamhuri.
“Kitendo cha Mahakama kutupa pingamizi za Polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni dalili njema kwetu. Tunaamini kesi hii tutashinda na hii ni aibu kubwa sana kwa Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla,” amesema Joyce Sokombi ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Mara
Naye Katibu wa Chadema Mkoa wa Geita, Rogers Luhega amesema wanaamini Mahakama itatenda haki katika kesi hiyo kwa kuruhusu marehemu Mawazo kuagwa kwa heshima kama inavyofanyika kwa wananchi wengine.
Polisi waondoa uzio Ofisi za Chadema
Kufuatia kuwepo kwa hali ya sintofahamu kuhusu mazishi ya marehemu Mawazo, polisi jana walilazimika kuwahi asubuhi Makao Makuu ya Ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, kisha kufungua na kuondoa uzio wa jeshi hilo uliokuwa umewekwa kwenye ofisi hizo.
Uzio huo uliwekwa kwenye Ofisi hizo za Chadema Kanda ya Ziwa kwa siku tatu kuanzia Jumapili iliyopita, ikiwa ni lengo la kuzuia waombolezaji kufika eneo hilo pamoja na kuzuia Mawazo asiagwe katika ofisi hizo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na baadaye mwandishi wetu kuthibitisha, zinaeleza kuwa askari polisi wafika kwenye ofisi hizo asubuhi ambapo walianza kazi ya kuondoa uzio huo ambao mara nyingi hutumika maeneo ya ‘hatari’.
Awali uzio huo uliowekwa siku ambayo polisi walizuia Mawazo kuagwa jijini Mwanza, ulisababisha kazi zote za chama hicho kusimama kutokana hali hiyo ambapo hata waombolezaji walizuiliwa kufika kwenye ofisi hizo kuhani msiba wa Mawazo.

IMETOKA MWANAHALISI ONLINE

WABUNGE WAMSHUKIA NDUGAI


112*Wadai amevunja kanuni Dk. Shein,  polisi kuingia ukumbini
*Kubenea naye atangaza kumburuza mahakamani
Fredy Azzah, Dar na Ramadhan Hassan, Dodoma
WABUNGE wa Chama cha Wananchi (CUF) wamemtuhumu Spika wa Bunge, Job Ndugai  kumruhusu Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein  kuingia bungeni.
Kwa mujibu wa wabunge hao, Spika alifanya bhivyo  licha ya wao kupinga hatua hiyo.
Vilevile, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), ametangaza kumfikisha mahakamani Spika Ndugai akidai kwamba alikiuka taratibu na kanuni za Bunge kwa kuwatoa nje wabunge wanaounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao pia wamemtuhumu  Ndugai kwa kuwaingiza katika ukumbi wa Bunge zaidi ya polisi 40 kinyume cha sheria.
Hayo waliyasema walipozungumza na waandishi wa habari   Makao Makuu ya CUF, Buguruni  Dar es Salaam jana.
Walisema katika hali ambayo hawakuitarajia, viti ambavyo hutumiwa na wabunge wa upinzani vilitolewa sehemu ya kukanyagia kwa hofu kwamba wangevitumia kuleta fujo.
Mwenyekiti wa wabunge hao, Juma Hamad Omar,   alisema kabla ya uzinduzi wa Bunge kufanywa na  Rais Dk. John Magufuli,   walimwandikia Spika Ndugai barua kuhusu msimamo wao wa kutotaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aingie ndani ya ukumbi wa Bunge.
Alisema licha ya kumwandikia barua pia  walipata fursa ya kufanya naye mazungumzo kwa takribani saa moja juu ya suala hilo.
Pamoja na juhudi zote hizo, Spika Ndugai alionekana kutotaka kuwasaidia akisema kuwa yeye uwezo wake ni  kumfikishia ujumbe Dk. Shein na kwamba mambo mengine hana uwezo nayo.
Juma alihoji kwa nini kiongozi huyo wa Bunge ashindwe kutumia mamlaka yake na badala yake afanye uamuzi kwa kushauriana na mhimili mwingine wa Serikali.
Alisema wabunge wa CCM Zanzibar walikataa Makamu wa Kwanza wa Rais wa visiwa hivyo, Maalimu Seif Sharif Hamad asiingie ndani ya ukumbi wa  Baraza la Wawakilishi siku baraza hilo lilipovunjwa na amri hiyo ilitekelezwa.
“Sasa yeye kwa nini ashindwe kutumia mamlaka yake na wakati wale ni waalikwa tu? Matokeo yake akaja kumuingiza mpaka Spika wa Baraza la Wawakilishi ambalo kwa sasa halipo.
“Na wakati akitengua kanuni ili hawa waingie, Tundu Lissu alipinga lakini spika kwa ubabe akapitisha,”alisema Juma.
Alisema kutokana na mambo hayo, Ndugai ndiye aliyemvunjia heshima Rais Dk. Magufuli kwa kushindwa kuwasikiliza wabunge wake ambao waliamua kupiga kelele na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Mnadhimu wa wabunge hao, Ali Salehe, alisisitiza    viongozi hao waliingizwa bungeni kinyume cha sheria.
Alisema  Spika bila kuwaombea kibali kama  kanuni zinavyotaka, aliruhusu zaidi ya polisi 40 kuingia ukumbini   lengo likiwa ni kupambana na wabunge wa upinzani.
Alisema baadhi ya askari hao walikuwa wamevaa sare na wengine walikuwa na nguo za raia na   walikuwa wamepangwa kila askari mmoja apambane na wabunge wanne wa upinzani.
“Lakini pia hata viti vya wapinzani na vile vya wabunge wa CCM vilikuwa tofauti.
“Kwenye vile vyetu walikuwa wametoa sehemu ya kuwekea miguu wakidhani tungeitumia kurusha wakati ambao tungefanya fujo kumbe sisi hatukuwa na mpango wa kufanya fujo,” alisema Salehe.
Wabunge hao walisema   Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  limezinduliwa na rais likiwa   halijakamilika.
Alisema kwa mujibu wa sheria Bunge hilo linatakiwa kuwa na wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi ambao mpaka sasa   hawapo kwa sababu uchaguzi wao umetangazwa kuahirishwa.
Kutokana na mambo hayo, wabunge hao walisema Zanzibar hakuna mgogoro wa siasa na kwamba CCM wanasema hivyo   kuhalalisha mambo yo.
“Kwa hiyo tunataka mchakato ukamilishwe na mshindi atangazwe ili pia kuhalalisha ushindi wa Dk. Magufuli ambaye alipigiwa kura na watu walewale waliompigia Maalimu Seif,” alisema.
Alisema   Wazanzibari wamechoka kusubiri, na kuendelea kuliweka taifa hilo kwenye taharuki ni kuhatarisha amani ya nchi.
MTANZANIA jana ilimtafuta Spika Ndugai kuzungumzia madai hayo lakini  hakupatikana.
Hata hivyo alipoulizwa, Ofisa habari wa Bunge, Owen Mwandumbiya, alipuuza madai ya wabunge hao kuhusu kilichotokea bungeni akisema wanajaribu kutengeneza kitu ambacho hakikuwapo.
Kubenea kutua kortini                           
Wakati huohuo,  Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, amesema anatarajia kumpeleka mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai akidai amekiuka taratibu na kanuni za Bunge kwa kuwatoa nje wabunge wanaounda Ukawa.
Akizungumza na waandishi wa habari   Dodoma jana, Kubenea alisema  Ndugai  alivunja kanuni na taratibu za Bunge kwa kuwatoa wabunge wa Ukawa nje kwa sababu  walichokuwa wakikidai ni halali.
Alisema kile walichokuwa wakikidai kuwa Rais wa Zanzibar Dk Shein hatakiwi kuingia bungeni ni kweli ikizingatiwa  aliingia Novemba 3 mwaka 2010 na ukomo wake ulikuwa ni 2 Novemba 2015.
“Spika anasema mpaka Rais atakapopatikana ndiyo unakuwa mwisho wa Rais wa Zanzibar, siyo kweli.
“Ukomo wa Rais wa Zanzibar uliishakoma na  katiba zetu za Tanzania na Zanzibar zinasema ndani ya miaka mitano au ukomo wa vipindi viwili visivyozidi miaka 10,’’ alisema.

Kubenea  alisema atampeleka mahakamani Ndugai akishirikiana na wakili wake, Peter Kibatara.
“Ndani ya wiki hii tunaenda mahakamani.  Job(Ndugai), amevunja taratibu na kanunu za bunge  na kulinajisi kwa kumruhusu Dk. Shein kuingia bungeni.
“Tunamshitaki kwa kuvunja kanuni na taratibu, tumeshauriana na mwanasheria wangu tunaenda mahakamani,’’ alisema
Mbunge huyo ambaye ni mwanahabari  mashuhuri, alishangazwa na hatua ya Spika Ndugai  kuwaruhusu Polisi na Usalama wa Taifa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu na kanuni zinazoendesha mhimili huo.
“Wale askari waliandaliwa kwa ajili ya kutupiga na walipania   kutupa mkong’oto.
“Sasa sisi tuna wabunge walemavu tuliogopa tukaamua kutoka nje, kitendo kile kimelivunjia hadhi Bunge   na nchi inayojiita yenye utawala bora.
“Nasema hivi Ndugai hana uwezo wa kulidhibiti Bunge wala kutuzuia sisi, tena tunamuonya mapema hawezi kuuzima huu moto huu,’’alisema Kubenea.

IMETOKA MTANZANIA

LOWASSA ALAKIWA NA MAELFU KAHAMA




WAZIRI mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amezua taharuki mjini Kahama, baada ya maelfu ya wananchi kujitokeza kumlaki. Anaandika Alli Litya, Kahama … (endelea).
“Mara baada ya kufika katika hospitali ya Kahama, ghafla uliibuka umati mkubwa wa wafuasi wa Ukawa, waliokuwa wamepeana taarifa kwa njia ya simu za mkononi juu ya ujio wa kiongozi wao,” anaeleza mmoja wa viongozi wandamizi wa UKAWA, mjini Kahama.
Lowassa, aliingia mjini Kahama kimyakimya mchana wa leo, ili kuwajulia hali wachimbaji wanne wa dhahabu waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Kahama.
Wachimbaji hao wamelazwa hosptalini hapo baada ya kufukiwa na vifusi kilichotokana na kuporomoka kwa udogo uliyofunika njia ya kuingia mgodini.
Mwanasiasa huyo anayeaminika kuwa ndiye aliyeshindi uchaguzi mkuu wa Oktoba, amefika hospitalini hapo na kutoa pole ya Sh. 2 milioni.
Katika safari hiyo, Lowassa aliambatana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba.
Makamba alilazimika kuwatuliza wananchi waliokuwa wakimshangilia Lowassa kwa kumuita rais na kuwaomba wasiwapigie kelele wagonjwa.
Aliwataka wamsubiri Lowassa atoke nje ya eneo la hospitali kwa kuwa safari yake ililenga kuwapa pole wagonjwa.
Akiwa katika wodi namba mbili ambayo waathirika wanne wamelazwa baada ya mwenzao mmoja Onyiwa Moris, kufariki dunia juzi, Lowassa aliwajulia hali waathirika na kisha kuwapa pole ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kila mmoja.
Amesema, anaungana na watanzania wengine kuwapa pole na kuwafariji na kwamba anaamini msaada huo aliowapa utawasaidia kwa matumizi mbalimbali wakiwa bado hospitali.
Joseph Burule, mmoja wa waathirika wa tukio hilo amesema, kufika kwa Lowassa kuwajulia hali, kumewapa faraja kubwa na kumewaongezea huzuni ya kukumbuka kuondokewa na mwenzao aliyefariki juzi saa sita mchana.
Burule ndiye mara baada ya kuzinduka alihoji kama Lowassa, ameshinda urais. Alipoambiwa aliyetangazwa kuwa mshindi, ni John Magufuli,alinyong’onyea na kuonyesha kuzidiwa na maradhi.
Hata hivyo, alionekana mchangamfu zaidi baada ya kumuona Lowassa na kudai kitendo cha kuwatembelea hospitalini hapo kimewapa moyo kwakuwa tangu waokolewe na kuanza kupatiwa matibabu, hakuna kiongozi hata mmoja aliyefika kuwajulia hali.
Wachimbaji hao wa madini, waliishi katika mashimo ya dhahabu kwa siku 41 na kuokolewa wote wakiwa hai.
Chacha Wambura alimueleza Lowassa kuwa hali zao hazijaridhisha hivyo anaiomba serikali iangalie uwezakano wa kuwahamishia katika hospiatli ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi zaidi.

IMETOKA MWANAHALISI 

Monday, 23 November 2015

MHE.LOWASSA AKIZUNGUMZIA SUALA LA JESHI LA POLISI KUWAZUIA KUUAGA MWILI WA MAWAZO

Familia ya Alphonce Mawazo walaani vikali kitendo cha jeshi la polisi ku...

UKAWA KUCHANGA MIL.33.9 KUSAIDIA FAMILIA YA MAWAZO

Ukawa kuchanga Mil 33.9 kusaidia familia ya Mawazo

WABUNGE wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamepanga kuchanga Sh. 33.9 milioni kwa ajili ya kusaidia familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoani wa Geita, Alfonce Mawazo. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Fedha, hizo zimepatika baada ya wabunge 113 wa Ukawa kuchangishana kiasi Sh. 300,000 kila mmoja ambazo zitakabidhiwa familia ya Mawazo ambaye ameuawa kikatili na watu ambao mpaka sasa hawajabainishwa.

Mwenyekiti wa Chadema – Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema hayo wakati akizungumza na mwanahalisionline mjini hapa Dodoma kuhusu maandalizi ya mazishi ya kada huyo ambaye anatajwa kuwa shujaa katika mapambado ya kutafuta ukombozi Ukawa.

Mbowe amesema licha ya kwamba Mawazo alikuwa mwanachama wa Chadema lakini pia alishiriki vyema katika ukombozi ndani ya Ukawa kwa kutetea masilahi ya Watanzania kwenye mkoa wake wa Geita pamoja na mikoa mingine nchini.

“Kwa ujumla wetu wabunge takribani 113 tumekubaliana kuchanga kiasi cha Sh. 300,000 kila mmoja kwa ajili ya kuiwezesha familia yake ambayo ameiacha.

“Kumbuka kwamba Mawazo amepigania masilahi ya Watanzania wengi katika mkoa wake wa Geita lakini pia katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Hivyo tunalazimika kumuenzi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wetu wa Ukawa na ikumbukwe kuwa, kwa sasa serikali ya CCM inaonesha wazi kutumia vyombo vyake vya dola kudidimiza upinzani,” amesema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe amesema inasikitisha kuona jeshi la polisi linavyotumiwa vibaya na kujikuta linafanya kazi za siasa badala ya kusimamia ulinzi na usalama wa raia.

“Leo (juzi), baada ya viongozi wa Mji wa Mwanza kupambana vikali na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, aliwaambia viongozi wa Chadema kuwa intelejensia imeonesha kuwa, iwapo watafanya mkusanyiko wa ibada kuna uwezekano wa kuzuka machafuko.

“Baada ya kupata taarifa hizo nilipata kuzungunza na IGP na kuniahaidi kunipatia majibu lakini hadi sasa sijafanikiwa kupata majibu lakini jambo lingine na la ajabu ni pale ambapo wamegeuza kibao na kusema hakuna kufanya ibada kwani kwa sasa kuna ugonjwa wa kipindupindu hivyo hakuna mkusanyiko,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema lazima Watanzania watambue kuwa serikali inatumia vibaya vyombo vyake vya dola kuzuia wapinzania wasifikishe ujumbe wao kwa jamii, imekifia hatua ya kuzuia hata watu kuwazika wafuasi wao.

“Sasa angalia kutuuwa wanatuuwa lakini hatua ya kutunyanyasa na kukataa hata tusimzike mtu wetu jambo hilo ni la ajabu sana lakini najua tutafikisha ujumbe kwa njia nyingine ambayo inafaa na kwa ustaarabu,” amesema Mbowe.



IMETOKA
Mwanahalisi Online

MAGUFULI AFUTA SHEREHE ZA KUADHIMISHA SIKU YA UHURU NCHINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI                   
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telegrams : "CABINET"
DAR ES SALAAM
Telephone : 2116898, 2116900/6
Fax : 2113425/2116914/2117272
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD
11400 DAR ES SALAAM.
Kwa mujibu wa  Sheria ya Sikukuu za Kitaifa  (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike  kwa kufanya kazi.  Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu  (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu.  Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi,  fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.

Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo,   sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23 Novemba, 2015
  

COPYRIGHT:nasmwanaharakati.blogspot.com