Tuesday, 24 November 2015

MAHAKAMA YAFYEKELEA MBALI PINGAMIZI LA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA LILE LA MKUU WA MKOA WA MWANZA







MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, jana ilishindwa kutoa maamuzi ya kesi iliyofunguliwa na familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita, Marehemu Alphonce Mawazo. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).
Kesi hiyo namba 10/2015 iliyopo chini ya Jaji, Lameck Mlacha, imefunguliwa juzi na familia hiyo ya Mawazo kwa lengo la kuomba tafsiri ya kisheria mahakamani hapo iwapo marehemu huyo hapaswi uzikwa kwa kuagwa kwa heshima kama wanavyoagwa binadamu wengine.
Awali leo mahakama hiyo ilisikiliza pande zote mbili za mlalamikaji na walalamikiwa, kisha kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa mahakamani na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kufuatia hali hiyo mahakama hiyo iliahirisha kwa muda kusikiliza shauri hilo kisha kutoa muda wa saa 1:30 kwa upande wa mlalamikaji ambayo ni familia ya Mawazo, kuwasilisha malalamiko muhimu mahakamani hapo.
Hata hivyo baadaye upande huo wa mlalamikaji uliwasilisha hoja hizo mahakamani hapo, ambapo Jaji Mlacha alidai baadhi ya vipengele vilikuwa havijakamilika, kwamba muda wa Mahakama hiyo pia ulikuwa umekwisha, hivyo kuipanga kesho kwa ajili ya kutoa maamuzi.
Hata hivyo, Jaji Mlacha aliwaacha solemba wananchi, wafuasia na viongozi wa Chadema baada ya kuamua kutolea maamuzi hayo sehemu nyingine mbali na Mahakama hiyo, hivyo kujikuta wananchi na wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamefurika kwa wingi mahakamani hapo wakipigwa butwaa.
Jaji Mlacha alitolea maamuzi hayo ya kuendelea kwa kesi hiyo kesho katika Ofisi yake iliyopo kwenye jengo la Mahakama Kuu ya Biashara Mkoa wa Mwanza.
Kesi yafunguliwa upya
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo leo jioni, mmoja wa mwanasheria wanaoitetea familia ya marehemu Mawazo, John Malya amesema familia hiyo imeamua kufungua kesi hiyo upya baada ya awali kuombwa na Mahakama hiyo kupeleka malalamiko mapya.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, kesi hiyo imefunguliwa tena leo kwa hati ya dharula ikiwa ni lengo la kuiomba Mahakama hiyo kutoa tafsiri ya kisheria kuhusu namna marehemu Mawazo anavyopaswa azikwe.
“Tunataka Mahakama itamke kwamba zuio lililowekwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (Charles Mkumbo) la kuzuia kuagwa Mawazo ni batili.
“Mahakama tunaiomba imkataze RPC kujihusisha na mazishi ya marehemu Alphonce Mawazo. Tunaamini Mahakama itatumia weledi wake kutenda haki katika kesi hii,” amesema mwanasheria Mallya.
Maamuzi ya awali
Awali Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ilitupilia mbali pingamizi mbili zilizowasilishwa mahakamani hapo baina ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza na Mwasheria Mkuu wa Serikali.
Pingamizi hizo zilidai mlalamikaji ambaye pia ni baba mdogo wa marehemu Mawazo, Charles Lugiko hana uhalali wa kisheria wa kutoa maombi hayo mahakamani, kwa kuwa yeye siyo baba mzazi wa marehemu Mawazo.
Kwamba hakuwasilisha mahakamani hapo hoja za kubishaniwa kwenye maombi hayo, jambo ambalo Jaji wa Mahakama hiyo, Lameck Mlacha aliziona pingamizi hizo zilizowasilishwa mahakamani hapo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hazina uzito kisheria.
Katika kesi hiyo namba 10/2015, familia ya marehemu Mawazo inawakilishwa na wanasheria wa Chadema ambao ni John Mallya, James Millya na Paul Kipeja, ambapo katika kujibu hoja hiyo ya upande wa walalamikiwa waliiambia Mahakama masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kupelekwa mahakamani.
Upande huo wa Jamhuri uliokuwa ukisimamiwa na wanasheria wawili, Seth Mkemwa na Emilly Kilia, awali ulidai kwamba mlalamikaji huyo hana uhalali wowote wa kupata ridhaa ya mahakama ya kumzika Mawazo, kwani hata katika maombi yake hajaonesha wazazi wa Mawazo kama wamefariki ama wapo hai.
Hata hivyo katika pingamizi hizo za awali, Jaji Mlacha alidai kwamba katika sheria namba 17 na 18 kifungu cha nne, vinaruhusu mtu yeyote aliyekuwa karibu na marehemu Mawazo anaweza kudai haki ya kumzika, kwani hata mila na desturi za kiafrika zinaeleza.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Jaji Mlacha, amesema kuwa hoja zinazotolewa na wanasheria wa Serikali wa kumpinga mlalamikaji kutosikilizwa mahakamani hazina tija, ambako alidai katika hati za mashitaka baba mdogo huyo alieleza kuwa alimlea na kumkuza hivyo anaowajibu wa kumzika
Upande wa mlalamikaji, uliokuwa ukitetewa na mawakili watatu, John Mallya, James Milya na Paul Kipeja, ulidai kuwa pingamizi za wanasheria wa Serikali ya kuomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo hazina msingi kwani mtu yeyote aliemlea marehemu anauwezo wa kuzika.
“Jaji amedai tupeleke maombi rasmi ya kutupilia mbali zuio la kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwaza Charles Mkumbo ya kuzuia kuagwa Mawazo hapa Mwanza, mambo tunayopeleka ni kutaka mahakama kutengua zuio la Polisi, Mahakama kumkataza RPC kutojihusisha na chochote kile kwenye kumuaga Mawazo,” alidai Mallya.
Mallya alidai kwamba katika maombi yao ya msingi wanayowasilisha mahakama ni ya kumzuia RPC Mkumbo kutojihusisha na chochote, huku akidai kwamba zoezi la kamanda huyo kuzuia uagaji lilikuwa ni batili na halikuwa halali.
Mbowe anena
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, akizungumza na umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza mahakamani hapo jana, ambapo aliwaomba wafuasi hao kuwa na subira kwani Mahakama itatoa uamuzi wakati wote wote.
Mbowe amesema Watanzania wote wakiwamo wapenda mabadiliko na watafuta haki nchini kuvuta subira kwani haki ya mtu haiwezi kunyang`anywa na watu wachache, kwa maslahi yao binafsi, kwani wana imani na Mahakama itatenda haki.
“Mpaka sasa tulipofikia tunaishukru Mahakama imeweza kufanya kazi yake. Tunaomba tuvumiliane na tuwe na subira, kwa sababu wanasheria wamepewa saa 1 na nusu wawe wamewasilisha maombi yao ya msingi ya kusikilizwa kesi hii na kutupilia mbali pingamizi wa wanansheria,” amesema Mbowe.
Watu wafurika mahakamani
Katika hatua nyingine, jana na leo maelfu ya wananchi walijitokeza kwa wingi kwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo la kikatiba, ambapo hata baada ya Mahakama kutupilia mbali pingamizi za Jamhuri, wananchi walionekana kushangilia kwa nguvu huku wakiimba nyimbo mbalimbali za chama hicho.
Pamoja na wananchi kujaa mahakamani hapo, maofisa wa Serikali wakiwamo askari polisi na maofisa wengine kutoka taasisi na idara za ulinzi na usalama nao walionekana kutanda kila mahala eneo hilo.
Askari polisi ambao wengi wao walikuwa wamevalia kiraia na wengine wakiwa na sare za jeshi hilo, walijaa mahakamani hapo kwa ajili ya kuimalisha ulinzi, ambapo hata hivyo hakuna vurugu zozote zilizotokea.
Baada ya Mahakama kutoa muda huo kwa upande wa walalamikaji kurekebisha baadhi ya vipengere vya kisheria, wananchi wengi wakiwamo wanawake, vijana na wazee walionekana kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama kutupilia mbali pingamizi hizo za RPC na AG.
Hata hivyo, wananchi hao wakiwamo wafuasi na viongozi mbalimbali wa Chadema walionekana kuwa watulivu baada ya Mwenyekiti Mbowe kuwasihi kupunguza munkari, hali iliyosababisha wengi wao kuanza kupongezana huku wakidai wameshinda kesi.
Baadhi ya viongozi na makada wa Chadema waliozungumza na MwanaHALISI Online kuhusu uamuzi huo wa awali, waliipongeza Mahakama kwa kutupilia mbali pingamizi hilo la upande wa Jamhuri.
“Kitendo cha Mahakama kutupa pingamizi za Polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni dalili njema kwetu. Tunaamini kesi hii tutashinda na hii ni aibu kubwa sana kwa Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla,” amesema Joyce Sokombi ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Mara
Naye Katibu wa Chadema Mkoa wa Geita, Rogers Luhega amesema wanaamini Mahakama itatenda haki katika kesi hiyo kwa kuruhusu marehemu Mawazo kuagwa kwa heshima kama inavyofanyika kwa wananchi wengine.
Polisi waondoa uzio Ofisi za Chadema
Kufuatia kuwepo kwa hali ya sintofahamu kuhusu mazishi ya marehemu Mawazo, polisi jana walilazimika kuwahi asubuhi Makao Makuu ya Ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, kisha kufungua na kuondoa uzio wa jeshi hilo uliokuwa umewekwa kwenye ofisi hizo.
Uzio huo uliwekwa kwenye Ofisi hizo za Chadema Kanda ya Ziwa kwa siku tatu kuanzia Jumapili iliyopita, ikiwa ni lengo la kuzuia waombolezaji kufika eneo hilo pamoja na kuzuia Mawazo asiagwe katika ofisi hizo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na baadaye mwandishi wetu kuthibitisha, zinaeleza kuwa askari polisi wafika kwenye ofisi hizo asubuhi ambapo walianza kazi ya kuondoa uzio huo ambao mara nyingi hutumika maeneo ya ‘hatari’.
Awali uzio huo uliowekwa siku ambayo polisi walizuia Mawazo kuagwa jijini Mwanza, ulisababisha kazi zote za chama hicho kusimama kutokana hali hiyo ambapo hata waombolezaji walizuiliwa kufika kwenye ofisi hizo kuhani msiba wa Mawazo.

IMETOKA MWANAHALISI ONLINE

No comments:

Post a Comment