Tuesday, 24 November 2015

WABUNGE WAMSHUKIA NDUGAI


112*Wadai amevunja kanuni Dk. Shein,  polisi kuingia ukumbini
*Kubenea naye atangaza kumburuza mahakamani
Fredy Azzah, Dar na Ramadhan Hassan, Dodoma
WABUNGE wa Chama cha Wananchi (CUF) wamemtuhumu Spika wa Bunge, Job Ndugai  kumruhusu Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein  kuingia bungeni.
Kwa mujibu wa wabunge hao, Spika alifanya bhivyo  licha ya wao kupinga hatua hiyo.
Vilevile, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), ametangaza kumfikisha mahakamani Spika Ndugai akidai kwamba alikiuka taratibu na kanuni za Bunge kwa kuwatoa nje wabunge wanaounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao pia wamemtuhumu  Ndugai kwa kuwaingiza katika ukumbi wa Bunge zaidi ya polisi 40 kinyume cha sheria.
Hayo waliyasema walipozungumza na waandishi wa habari   Makao Makuu ya CUF, Buguruni  Dar es Salaam jana.
Walisema katika hali ambayo hawakuitarajia, viti ambavyo hutumiwa na wabunge wa upinzani vilitolewa sehemu ya kukanyagia kwa hofu kwamba wangevitumia kuleta fujo.
Mwenyekiti wa wabunge hao, Juma Hamad Omar,   alisema kabla ya uzinduzi wa Bunge kufanywa na  Rais Dk. John Magufuli,   walimwandikia Spika Ndugai barua kuhusu msimamo wao wa kutotaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aingie ndani ya ukumbi wa Bunge.
Alisema licha ya kumwandikia barua pia  walipata fursa ya kufanya naye mazungumzo kwa takribani saa moja juu ya suala hilo.
Pamoja na juhudi zote hizo, Spika Ndugai alionekana kutotaka kuwasaidia akisema kuwa yeye uwezo wake ni  kumfikishia ujumbe Dk. Shein na kwamba mambo mengine hana uwezo nayo.
Juma alihoji kwa nini kiongozi huyo wa Bunge ashindwe kutumia mamlaka yake na badala yake afanye uamuzi kwa kushauriana na mhimili mwingine wa Serikali.
Alisema wabunge wa CCM Zanzibar walikataa Makamu wa Kwanza wa Rais wa visiwa hivyo, Maalimu Seif Sharif Hamad asiingie ndani ya ukumbi wa  Baraza la Wawakilishi siku baraza hilo lilipovunjwa na amri hiyo ilitekelezwa.
“Sasa yeye kwa nini ashindwe kutumia mamlaka yake na wakati wale ni waalikwa tu? Matokeo yake akaja kumuingiza mpaka Spika wa Baraza la Wawakilishi ambalo kwa sasa halipo.
“Na wakati akitengua kanuni ili hawa waingie, Tundu Lissu alipinga lakini spika kwa ubabe akapitisha,”alisema Juma.
Alisema kutokana na mambo hayo, Ndugai ndiye aliyemvunjia heshima Rais Dk. Magufuli kwa kushindwa kuwasikiliza wabunge wake ambao waliamua kupiga kelele na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Mnadhimu wa wabunge hao, Ali Salehe, alisisitiza    viongozi hao waliingizwa bungeni kinyume cha sheria.
Alisema  Spika bila kuwaombea kibali kama  kanuni zinavyotaka, aliruhusu zaidi ya polisi 40 kuingia ukumbini   lengo likiwa ni kupambana na wabunge wa upinzani.
Alisema baadhi ya askari hao walikuwa wamevaa sare na wengine walikuwa na nguo za raia na   walikuwa wamepangwa kila askari mmoja apambane na wabunge wanne wa upinzani.
“Lakini pia hata viti vya wapinzani na vile vya wabunge wa CCM vilikuwa tofauti.
“Kwenye vile vyetu walikuwa wametoa sehemu ya kuwekea miguu wakidhani tungeitumia kurusha wakati ambao tungefanya fujo kumbe sisi hatukuwa na mpango wa kufanya fujo,” alisema Salehe.
Wabunge hao walisema   Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  limezinduliwa na rais likiwa   halijakamilika.
Alisema kwa mujibu wa sheria Bunge hilo linatakiwa kuwa na wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi ambao mpaka sasa   hawapo kwa sababu uchaguzi wao umetangazwa kuahirishwa.
Kutokana na mambo hayo, wabunge hao walisema Zanzibar hakuna mgogoro wa siasa na kwamba CCM wanasema hivyo   kuhalalisha mambo yo.
“Kwa hiyo tunataka mchakato ukamilishwe na mshindi atangazwe ili pia kuhalalisha ushindi wa Dk. Magufuli ambaye alipigiwa kura na watu walewale waliompigia Maalimu Seif,” alisema.
Alisema   Wazanzibari wamechoka kusubiri, na kuendelea kuliweka taifa hilo kwenye taharuki ni kuhatarisha amani ya nchi.
MTANZANIA jana ilimtafuta Spika Ndugai kuzungumzia madai hayo lakini  hakupatikana.
Hata hivyo alipoulizwa, Ofisa habari wa Bunge, Owen Mwandumbiya, alipuuza madai ya wabunge hao kuhusu kilichotokea bungeni akisema wanajaribu kutengeneza kitu ambacho hakikuwapo.
Kubenea kutua kortini                           
Wakati huohuo,  Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, amesema anatarajia kumpeleka mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai akidai amekiuka taratibu na kanuni za Bunge kwa kuwatoa nje wabunge wanaounda Ukawa.
Akizungumza na waandishi wa habari   Dodoma jana, Kubenea alisema  Ndugai  alivunja kanuni na taratibu za Bunge kwa kuwatoa wabunge wa Ukawa nje kwa sababu  walichokuwa wakikidai ni halali.
Alisema kile walichokuwa wakikidai kuwa Rais wa Zanzibar Dk Shein hatakiwi kuingia bungeni ni kweli ikizingatiwa  aliingia Novemba 3 mwaka 2010 na ukomo wake ulikuwa ni 2 Novemba 2015.
“Spika anasema mpaka Rais atakapopatikana ndiyo unakuwa mwisho wa Rais wa Zanzibar, siyo kweli.
“Ukomo wa Rais wa Zanzibar uliishakoma na  katiba zetu za Tanzania na Zanzibar zinasema ndani ya miaka mitano au ukomo wa vipindi viwili visivyozidi miaka 10,’’ alisema.

Kubenea  alisema atampeleka mahakamani Ndugai akishirikiana na wakili wake, Peter Kibatara.
“Ndani ya wiki hii tunaenda mahakamani.  Job(Ndugai), amevunja taratibu na kanunu za bunge  na kulinajisi kwa kumruhusu Dk. Shein kuingia bungeni.
“Tunamshitaki kwa kuvunja kanuni na taratibu, tumeshauriana na mwanasheria wangu tunaenda mahakamani,’’ alisema
Mbunge huyo ambaye ni mwanahabari  mashuhuri, alishangazwa na hatua ya Spika Ndugai  kuwaruhusu Polisi na Usalama wa Taifa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu na kanuni zinazoendesha mhimili huo.
“Wale askari waliandaliwa kwa ajili ya kutupiga na walipania   kutupa mkong’oto.
“Sasa sisi tuna wabunge walemavu tuliogopa tukaamua kutoka nje, kitendo kile kimelivunjia hadhi Bunge   na nchi inayojiita yenye utawala bora.
“Nasema hivi Ndugai hana uwezo wa kulidhibiti Bunge wala kutuzuia sisi, tena tunamuonya mapema hawezi kuuzima huu moto huu,’’alisema Kubenea.

IMETOKA MTANZANIA

No comments:

Post a Comment